Dc Chemba alaani vikali unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya jamii Nchini kwa madai kuwa ni tamaduni zao.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mh.Simon Odunga amelaani vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia hasa Ukeketaji unaoendelea kufanywa na baadhi ya jamii Nchini kwa madai kuwa ni tamaduni zao.
Amekea vitendo hivyo baada ya kuripotiwa kesi mbalimbali katika Idara za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Wilayani Chemba zikihusisha unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike na zingine kushudia kwa macho ikiwamo ya binti wa miaka 13 kuolewa na mzee wa miaka 47 majuma machache yaliyopita.
Aidha Mh.Odunga amenukuliwa akisema kuwa “Yeyote katika Wilaya ya Chemba atakaeripotowa kuhusika na namna yeyote ya unyanyasaji wa kijinsia iwe kwa kukeketa au kujihusisha na ndoa za kuolewa/kuoa watoto wadogo wenye umri wa kwenda shule,hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufungwa jela”
Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Wilaya ya Chemba amezishukuru Idara za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na serikali za vijiji kwa kuendelea kubainisha maovu yanayofanywa na baadhi ya jamii ndani ya Wilaya ya Chemba ambapo ameziomba idara hizo kuendelea kuibua maovu mbalimbali kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Sanjari na hayo Mh.Odunga amewaomba Wananchi wote Wilayani Chemba kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kuzifichua jamii zinazokumbatia mila na tamaduni zisizokubalika katika jamii mara tu baada ya kuwabaini ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho kwa jamii zingine.

No comments