HABARI: Familia ya Ndesamburo yatimza ahadi ya Baba yao kwa Familia za wanafunzi wa Lucky Vicent waliopata ajali May 6 mwaka jana
Hatimaye Familia ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Moshi Mjini marehemu ,Phillemon Ndesamburo imekabidhi kiasi cha sh,3 milioni kama ahadi ya rambirambi iliyotolewa na marehemu kabla ya kufariki dunia kwa wahanga wa tukio la ajali ya basi lililoua wanafunzi na watumishi wa shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha.
Marehemu Ndesamburo kabla ya kuaga dunia Mei 31 mwaka jana alihaidi kutoa rambirambi kwa ajili ya wahanga wa ajali hiyo lakini kabla ya kutimiza ahadi yake aliaga dunia baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake mjini Moshi.
Tukio la kukabidhi rambirambi hiyo lilienda sambamba na zoezi la kutembelea mnara wa kumbukumbu wa wanafunzi 32,walimu 2 pamoja na dereva mmoja waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea mwaka jana katika eneo la Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha .
Akizungumza mapema Leo Juni 5 mwaka huu,mara baada ya kukabidhi rambirambi huyo, Rita Thadey ambaye ni mtoto wa marehemu Ndesamburo alisema kwamba kwa muda mrefu alikuwa akiumizwa na ahadi ya marehemu baba yake lakini leo anamshukuru mungu kwa kutimiza na wanajiona wapo huru sasa
“Sisi kama familia tumejisikia faraja sana kutimiza ahadi iliyoachwa na marehemu baba yetu ni hilo tu”alisema Rita
Meya wa jiji la Arusha,Kalist Lazaro alisema kwamba marehemu Ndesamburo siku chache kabla ya kuaga dunia alimpigia simu na kumwita nyumbani kwake ili aweze kumkabidhi rambirambi na alipomfuata nyumbani hali yake ilibadilika ghafla kabla ya kuaga dunia.
Lazaro alisema kwamba marehemu Ndesamburo alifariki akiwa mikononi mwake lakini anajisikia faraja mara baada ya familia ya marehemu kuhakikisha wanatimiza ndoto na ahadi yake.
“Ahadi hii ilikuwa niipokee mimi kwa kuwa marehemu aliniita nyumbani kwake anikabidhi rambirambi lakini nilipowasili hali yake ya afya ilibadilika ghafla na akafariki mikononi mwangu”alisema Lazaro
Akipokea rambirambi hiyo kwa niaba ya wahanga wa tukio hilo,Roland Mwalyambi alisema kwamba wanashukuru kwa kupokea ahadi iliyoachwa na marehemu Ndesamburo na kusisitiza ya kwamba hawana cha kulipa zaidi ya kuwaombea mema waliojitolea.
No comments