Serikali imewasisitiza wananchi kuacha matumizi ya mkaa na badala yake watumie nishati nyingine ili kuepuka changamoto za uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kote nchini kutokana na matumizi ya mkaa.
Msisitizo huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika Juni 5 mwaka huu.
Waziri Makamba alisema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapa fursa wananchi wa Jiji la Da re Salaam kuelimishwa na kuhamasishwa kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaolikumba jiji hilo ikiwemo mafuriko, uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki, kubomoka kwa kuta za fukwe za Bahari ya Hindi pamoja na utumiaji wa kiasi kikubwa cha nishati ya mkaa.
“Nasisitiza kwamba, sote tuna jukumu la kuanza kubadilika kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuanza kutumia nishati mbadala wa mkaa. Tukumbuke kwamba suala la kuhifadhi mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo,” alisema Makamba.
Waziri Makamba alieleza kuwa matumizi makubwa ya mkaa hayapo tu katika Jiji la Dar es Salaam bali pia yapo katika maeneo mengine ya nchi, hivyo kutokana na matumizi makubwa ya nishati hiyo, maadhimisho ya kitaifa yataongozwa na Kaulimbiu inayosema; “Mkaa Gharama; Tumia Nishati Mbadala”.
No comments