Shilingi 1000 yafanya mke akatwe Koromeo
Mwananke mmoja aliyefahamika kwa jina la Mary Miyombo, mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa mtaa wa Zepisa Kata ya Hombolo bwawani katika Jiji la Dodoma amenusurika kufa baada ya kukatwa koo (Koromeo) na mume wake kwa wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limetokea Mei 16 mwaka huu mnamo majira ya saa 6 usiku ambapo inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikutwa akiwa na mwanaume mwingine ndipo mmewe ajulikanye kwa jina la Mgowela Andasoni akamjeruhi kwa kumkata na Panga kwenye koo na kisha kukimbia.
Akielezea tukio hilo Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Zepisa Albina Amon amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba yeye alichukua hatua za kuhakikisha mwanamke huyo anapata tiba.
Mtendaji huyo alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa sita usiku katika nyumba anayoishi mwanamke huyo.
Akisimulia zaidi alisema kuwa baada ya mtuhumiwa kufanya tukio hilo alikimbilia kusikojulikana lakini juhudi za kumtafuta ziliendelea ambapo majira ya saa kumi na moja alfajili alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Hombolo.
“Nimesikitishwa sana na ukatili unaoendelea kufanywa na wanaume dhidi ya wanawake nahasa kuwapiga mara kwa mara na kuwajeruhi ilihali juzi tu tumetoka kuadhimisha siku ya familia duniani”alisema Amoni.
Aidha aliiambia Darmpya.com kuwa mtuhumiwa huyo ambaye yupo lupango kwa sasa aliwahi kumpiga mama yake mzazi katika kipindi cha mwaka 2015 na akafungwa jela.
Pia Darmpya.com ilifika katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo iliweza kuongea na mama huyo aliyejeruhiwa kwa panga na mumewe.
Akizungumza kwa taabu sana mama huyo huku akilia alisema kuwa mwanaume huyo aliyemjeruhi hakuwa mume wake ila ni hawara yake tu kwani anamke wake.
Alisema ikiwa majira ya saa 7 mchana akitokea kuuza pombe kilabuni kijijini hapo alifika nyumbani kwake nakwenda anapowekaga hela zake ambapo aligundua elfu moja haipo jambo lililosababisha kumuuliza mume wake.
Alisema alipomuuliza mumewe kama amechukua hela hiyo ndipo kipigo kilipoanza hadi kufikia hatua ya kukatwa na panga shingoni.
“Yani simtaki tena yule mwanaume kwani hii ni mara ya tatu ananipiga na kunijeruhi na nimekuwa nikimsamehe lakini kwa hili simtaki tena” alisema Merry.
“Wazazi wangu wote walisha fariki nimebaki na bibi ambaye naye nimzee sana na ananitegemea kwani sina ndugu mwingine zaidi yake” alisema.
Naye Diwani wa kata ya Hombolo Bwawani Ased Ndajiro alisema kuwa anataarifa ya tukio hilo nakusema kuwa kwa taarifa alizonazo mama huyo alifumaniwa na mume akiwa na mwanaume mwingine ndipo mwanaume huyo alipoajichukulia hatua mkononi kwa kumkata na panga.
Alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na hayo matukio ili isijekuonekana wanawake wanaonewa wakati mengine wanayazua wao.
“Watu wanatakiwa kupunguza mihemko yao jamani sasa mtu ameolewa lakini bado anachepuka anatarajia nini”, alisema.
Hata hivyo Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma Dkt. Caloline Damian alithibitisha kumpokea mgonjwa huyo hospitalini hapo ambapo alifanyiwa oparesheni na kulazwa wodi namba 10.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji kwa sasa hali ya mgonjwa inaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa hapo awali” alisema Damian.
Aidha Darmpya.com ilimtafuta Kamanda wa polisi Gilles Muroto kuzungumzia tukio hilo ambapo alisema hana taarifa hizo lakini atafuatilia.
No comments