DC Mbulu auvunja Uongozi wa Kijiji
UONGOZI wa serikali ya kijiji cha Tumati, umevunjwa kutokana na kusababisha migogoro kati yao na wananchi kwa miaka minne sasa
Uamuzi wa kuvunja uongozi huo, ulitolewa na mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, katika mkutano wake alioufanya kijijini hapo juzi
Uamuzi wa kuvunja uongozi huo, ulitolewa na mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, katika mkutano wake alioufanya kijijini hapo juzi
Serikali ya kijiji hicho ilikuwa ikiongozwa na mwenyekiti Ezekiel Martin (Chadema), lakini tangu mwaka 2015, kumekuwa na migogoro isiyoisha kati ya viongozi na wananchi.
|
Baada ya kuvunja uongozi, Mofuga, alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga, kuitisha upya uchaguzi wa kijiji hicho.
|
Alisema hawezi kukubali kuona wananchi wanalalamikia serikali ya kijiji inayoongozwa na mwenyekiti wao naye asichukue hatua kwa faida ya jamii.
“Malalamiko mengi yametolewa na wananchi dhidi ya viongozi wao wakisema wanasababisha migogoro kila wakati, ni heri waondoke ili wachaguliwe viongozi wengine,” alisema.
Alisema wananchi wanahitaji viongozi ambao watawaongoza ili wapate maendeleo na siyo kupewa vitisho na kuibua migogoro.
“Wakae pembeni na kuwapisha wengine, kwa kuwa wameshindwa kazi,” alisema.
Mapema katika mkutano huo baadhi ya wananchi waliwalalamikia viongozi wa kijiji hicho kuwa wanawanyanyasa kupitia uongozi wao hivyo kuwataka waondoke madarakani.
Mkazi wa kijiji hicho, Elias Boay alisema, viongozi hao wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi na kuongoza kibabe.
"Katika kijiji chetu hakuna utawala bora unaofanyika zaidi ya udikteta kwani uongozi umekuwa ukiwaweka rumande baadhi ya wananchi chumba kimoja bila kujali jinsia yao,” alisema.
Alisema uongozi huo ulikuwa hausikilizi kero za wananchi na wajumbe wa serikali ya Kijiji walikuwa wanawatoza watu faini bila kutoa risiti.
Mkazi mwingine, Magdalena Ombay, alisema iwapo mkurugenzi wa halmashauri ataitisha uchaguzi mwingine, wanatarajia kuchagua viongozi bora watakaowaongoza vyema na kuachana na kelele za kila siku.
Hata hivyo, kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji hicho, Martin alisema, kuvunjwa kwa uongozi wake, kumetokana na siasa na siyo kwa sababu ya utendaji wao kuwa mbaya.
“Siasa zimeingizwa katika hili suala kwa sababu ya itikadi ya Chadema niliyonayo.
"Hii mizengwe ilikuwa tangu siku nyingi hata Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alipofanya ziara yake Mbulu na kufika hapa kijijini baadhi ya watu walimwambia majungu," alisema.
No comments